Monday, May 14, 2012

Mkurugenzi Magu akiri kulipa mishahara marehemu

HATIMAYE Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, imekiri kuwepo kwa ufisadi mkubwa wa kulipa mishahara hewa, ikiwemo ya watumishi wake waliostaafu na wale waliofariki dunia.
Kutokana na ukweli huo, halmashauri hiyo tayari imemsimamisha kazi mtumishi wake aliyekuwa anahusika na ulipaji wa mishahara watumishi, Anjelina Kamugisha, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo nzito za ufisadi.
Imeelezwa kwamba, baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ya Magu ambao kwa sasa ni marehemu pamoja na watumishi waliostaafu kazi, kwa muda mwingi wamekuwa wakiingiziwa malipo ya mishahara yao kwenye benki ya NMB tawi la Magu, kisha fedha hizo kutolewa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa benki hiyo wasio waaminifu.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ya Magu, Cornel Ngudungi (DED), aliyathibitisha hayo jana jioni, wakati alipokuwa akitoa taarifa ya  tuhuma za ubadhilifu huo, katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani, kilichoketi chini ya mwenyekiti wake, Boniventure Kiswaga mjini humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Boniventure Kiswaga
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, Boniventure Kiswaga (katikati aliyesimama), akituliza munkari ya madiwani kuhusu marehemu kulipwa mishahara na halmashauri hiyo. Kulia kwake Mwenyekiti ni Mkurugenzi mwenyewe (aliyevaa tai)
“Mheshimiwa mwenyekiti, taarifa za halmashauri kulipa mishahara kwa marehemu na wastaafu, ni kweli zipo. Nimelazimika kuzifuatilia hadi kwa uongozi wa NMB.
“Mishahara hii ilikuwa ikiingizwa benki ya NMB tawi la hapa Magu. Baada ya kuingizwa ilikuwa ikitolewa na baadhi ya watumishi wetu kwa kushirikiana na wale wa benki wasiowaaminifu.
“Kwa hiyo, nimeamua kumsimamisha kazi Anjelina Kamugisha ambaye ndiye aliyekuwa anasimamia ulipwaji wa mishahara. Tuhuma hizi za mishahara hewa zipo na tunazifanyia kazi”, alisema Mkurugenzi Ngudungi bila kutaja idadi ya fedha za mishahara hewa zilizolipwa.
Madiwani wa Halmashauri ya Magu wakifuatilia mjadala
Madiwani wa Halmashauri ya Magu wakifuatilia mjadala mkali wa halmashauri hiyo kulipa mishahara kwa watumishi wa halmashauri hiyo ambao walishafariki dunia na wale waliostaafu kazi
Inasadikiwa kwamba, halmashauri hiyo imetumia mamilioni ya fedha kulipa mishahara hewa kwa wastaafu na watumishi wake waliotangulia mbele ya haki, na Sifa Zivume itaendelea kuchokonoa kiundani zaidi ili kubaini idadi halisi ya fedha hizo zilizotumika vibaya.
Aidha alieleza kwamba, ili kubaini ukweli wa mambo, yeye alilazimika kuonana na uongozi wa NMB tawi hilo la Magu, kwa lengo jema la kupata usahihi wa taarifa hizo, lakini aliombwa aende jijini Mwanza akaonane na Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa.
Alisema, baada ya kuonana na meneja huyo aliyemtaja kwa jina la Chilongola, alielezwa kwamba, benki hiyo haiwezi kutoa fedha hizo mpaka vyombo vya dola, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), na jeshi la polisi waamue kutolewa kwa fedha hizo na si vinginevyo.
“Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Bwana Chilongola aliniambia hawawezi kuzungumzia suala hilo hadi wapeleke barua.
“Na tulipopeleka barua alitujibu benki yake haiwezi kutoa fedha hizo mpaka TAKUKURU au polisi waamuru kutolewa kwa fedha hizo”, alifafanua Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya hiyo ya Magu, huku akimuonesha mwenyekiti Kiswaga majibu ya barua ya NMB.
Alisema, tayari alishamwandikia barua Mkuu wa kituo cha Polisi wilaya hiyo ya Magu, akimuomba asaidie kupata taarifa ya ripoti ya ukaguzi wa NMB, na kwamba amemuagiza Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo aanze mara moja ukaguzi wa wizi huo, pamoja na kutoa ushirikiano zikiwemo nyaraka zote kwa Mkaguzi.
Awali, kulikuwepo na taarifa za halmashauri hiyo kulipa mishahara hewa, ikiwemo ya watu waliofariki dunia na wale waliostaafu kazi katika halmashauri hiyo, lakini ukweli wake ulikuwa haujabainika.
Taarifa hiyo, imekuja kufuatia kikao kilichopita cha baraza la madiwani wa Magu, ambacho kilitoa maazimio ya kuitaka ofisi ya Mkurugenzi kufuatilia tuhuma hizo, na kikao cha juzi atoe taarifa ya tuhuma hizo za ubadhilifu wa mali ya umma.
Licha ya Mkurugenzi Ngudungi kutoa taarifa hiyo ya utekelezaji wa baraza la madiwani, lakini madiwani wenyewe walichachamaa na kumtaka Mkurugenzi huyo aeleze kwa nini nani aliyekuwa anaidhinisha mishahara ya watumishi, ikiwemo mishahara hiyo hewa.
Diwani wa Kata ya Lubugu, Julius Ngongoseke (UDP), alisimama na kumtaka Mkurugenzi Ngudungi alieleze baraza hilo kama kuna mtu tofauti na Mkurugenzi anayeidhinisha kulipwa kwa mishahara hiyo.
Kufuatia hali hiyo ya vuta ni kuvute, mwenyekiti wa halmashauri hiyoanayesifiwa kwa umakini katika kazi zake, alilazimika kuvunja kanuni kisha kusimama kikaoni na kuwaomba madiwani wasiendelee kulijadili suala hilo, kwani kufanya hivyo wanaweza kutoa fursa ya mtuhumiwa kulalamika kwamba amejadiliwa mapema, hivyo liachwe lishughulikiwe kisheria zaidi.

No comments:

Post a Comment